Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Bw. Dioniz Malinzi, amezindua rasmi mbio za Rock City Marathon, zitakazofanyika Oktoba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza katika uzinduzi huo jana jijini Dar es Salaam, Malinzi alisema mbio hizo zimeweza kuwa ni moja ya mbio zinazoheshimika nchini Tanzania na kuiweka kanda ya ziwa katika kalenda ya michezo kila mwaka.
Malinzi aliipongeza kampuni ya Capital Plus International (CPI) kwa kuendelea kujidhatiti katika maandalizi ya mbio hizo na kuziboresha kila mwaka licha ya changamoto nyingi zinazoukabili mchezo huo wa riadha nchini.
“Ni kweli kwamba makampuni na hata watu binafsi wamekuwa wakisaidia kukuza mchezo wa riadha hapa nchini, lakini bado mchezo huu unachangamoto nyingi.
“Jitihada za pamoja zinahitajika baina ya serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, sisi Baraza la Michezo la Taifa (BMT), vyama vya michezo, mashirika na wadau wengine, ili kurejesha heshima iliyopotea miongoni mwa michezo na wanamichezo wa Tanzania, hususani riadha,” alisema Bw. Malinzi.
Bw. Malinzi alibainisha kuwa na kuwepo kwa changamoto mbali mbali CPI imekuwa ikijitahidi kuboresha mbio hizo zifanyikazo kila mwaka.
“Tumeshuhudia viwango vya mbio hizi vikipanda kila mwaka, ambapo ni kielelezo cha maandalizi mazuri yanayofanywa kwa kuzingatia viwango na sheria zilizo wekwa,” aliongeza Bw. Malinzi.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa BMT alisisitiza kuwa vyama vya michezo pia vinapaswa kujiimarisha katika kuwaandaa wachezaji kabla ya kuwapeleka kushiriki katika mashindano ya kimataifa ambapo wachezaji hao wanabeba jina la nchi ya Tanzania.
“Hatunabudi kuimarisha msingi wetu katika kila aina ya michezo hapa nchini, kama bado tunayo ndoto ya kuirudisha ramani ya Tanzania katika ulimwengu wa michezo kama ilivyokuwa zamani,” alisisitiza.
Tukio hilo limewavutia wadau wengi wa michezo nchini, ikiwa ni pamoja na makampuni makubwa kama Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Kampuni ya TSN Group Ltd, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers, Mfuko wa Pensions (PPF), Sahara Communication, ATCL, New Mwanza Hotel, na New Africa Hotel ambao wamejitokeza kudhamini mbio hizo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya Capital Plus International, Bw. Mathew Kasonta, alisema mbio za mwaka huu zitahusisha mbio za nusu Marathon za kilomita 21, mbio za kujifurahisha maarufu kama Corporate Race za kilomita 5, mbio za watu wenye ulemavu wa ngozi za kilomita 3, mbio za watu wazima za kilomita 3 na mbio za watoto kuanzia miaka saba hadi 10 ambazo ni za kilomita 2.
Bw. Kasonta alisema kuwa mbio hizo zinaenda sambamba na kuhamasisha Utalii wa ndani kupitia sekta ya michezo, ambapo washiriki watakua ni kutoka kanda ya ziwa Victoria na nchi jirani kama Kenya, Uganda, Afrika Kusini na baadhi yao wakiwa na uzoefu wa kucheza mashindano ya kimataifa ili kutoa ushindani zaidi.
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wafadhili mbalimbali wanaoshirikiana nasi ili kuyafanikisha mashindano haya, kwa niaba ya Capital Plus International, ningependa kuwahakikishia kuwa mashindano ya mwaka huu yataboreshwa zaidi na hivyo yataweza kutupatia wanariadha bora watakaoiwakilisha nchi yetu kikamirifu katika mashindano ya kimataifa,” alisema Bw. Kasonta.