Monday 9 June 2014

Mbio za Rock City Marathon 2013 zafana

Na Mwandishi wetu
WANARIADHA Alphonce Felix kutoka Arusha na Vicoty Chepkemoi kutoka Kenya wameibuka vinara katika mashindano ya riadha ya kilometa 21 yanayojulikana kama ‘Rock City Marathon 2013’ yaliyofanyika Jijini Mwanza jana Jumapili nakujinyakulia Shilingi milioni moja na nusu (Sh 1.5 m) kila mmoja.
Alphonce alishinda mbio hizo kwa upande wa wanaume baada ya kutumia saa 1:02:17 hivyo kuvunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na mwanariadha Kopiro Chacha aliyetumia 1:05:00, huku Chepkemoi aki kutumia 1:12:44.
Nafasi ya pili alishika Joel Kimtiae wa Kenya kwa upande wa wanaume na Sarah Ramdhani kutoka Arusha kwa upande wa wanawake, wakifuatiwa na Sambo Andrea kwa upande wa wanaume na Zakia Mrisho kwa upande wa wanawake wote wakitokea Tanzania.
Zaidi ya wanariadha 1090 walijitokeza kushiriki mashindano hayo yanayoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International kwa mwaka wa tano mfululizo.
Wambura Lameck kutoka Holili alingara katika mbio za kilometa tano huku Dotto Ikangaa kutoka Arusha akishika nafasi ya pili .

Kwa mujibu wa waratibu wa mbio hizi, udhamini waliopata kutoka kwa wadamini ambao ni, Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), Africa Barrick Gold (ABG), Precision Air, Airtel kupitia Airtel Money, TANAPA, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza Hotel, Sahara Communications, Continental Decoders na Umoja Switch, umewawezesha kuboresha tuzo kwa washiriki pamoja na kufanya maadalizi mazuri yanayozingatia sheria za riadha.
Washiriki na washabiki wa mbio za Rock City za mwaka huu walipata kuburudishwa na kikundi cha Sanaa cha Bujora ambacho kilionyesha umahiri wake wa kuonyesha utamaduni wa kitanzania kupitia dansi.         
Mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw Kizito Bahati (Afisa michezo Manispaa ya Ilemela), mbali na kutaka washiriki kutoka kanda ya ziwa kuchangamkia fursa inayoletwa na mbio hizo, pia aliwataka viongozi wa vyama vya riadha kuwa na program endelevu ya kukuza mchezo wa riadha kwa kushirikiana na Maafisa Michezo wa Mikoa na Wilaya ili waweze kupata fursa ya kufikisha na kuufundisha mchezo huu katika shule ambako ndio chimbuko la vipaji vya michezo.
“Nawashukuru sana waandaaji wa mbio hizi za Rock City Marathon kwa kuweza kuandaa shindano ambalo limeweza kutusaidia sisi wadau wa riadha kugundua vipaji vingi ambavyo tunavyo hapa nchini. Hivi vipaji vinastahili kukuzwa. Hivyo basi natoa wito kwa watu wote wenye dhamana ya michezo kutumia mbio hizi kama chambo cha kuweza kutambua vipaji vingi vya riadha ambavyo vinahitaji kuendelezwa kwa manufaa ya taifa,” alisema Bw Kizito.
Pamoja na hayo mashindano haya yameweza kufanikiwa kwa udhamini wa makampuni mbalimbali nayapongeza kwa juhudi zao za kuweza kuinua michezo hapa mkoani Mwanza na Tanzania kwa ujumla. Nayaomba na makampuni mengine kujitokeza kudhamini michezo hii kwani fursa kwao katika kutangaza bidhaa zao.

Mshindi  wa kwanza wa mbio za Rock City Marathon 2013 kilomita 21 kwa upande wa wanaume Alphonse Felix kutoka mkoani Arusha akimalizia mbio hizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba ambapo alitumia saa 1:02:17 na kufanikiwa kuvunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na Opio Chacha aliyetumia saa 1:05:47.

Powered by Blogger.