Na Mwandishi
Wetu
UZINDUZI wa
msimu wa sita wa mbio za Rock City Marathon 2014 zilizoanza mwaka 2009, zikiwa
na lengo la kukuza Utalii wa Ndani kupitia michezo, unatarajia kufanyika
Septemba 10, kwenye Hoteli ya New Afrika, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa mbio hizo, Bi. Grace Sanga, alisema kuwa
baadhi ya wanariadha, viongozi wa vyama vya riadha, viongozi wa Baraza la
Michezo Tanzania na wadau mbali mbali wa mchezo wa riadha nchini wanatarajiwa
kuhudhuria uzinduzi huo.
Bi. Grace
alisema kuwa pamoja na maandalizi ya mbio za mwaka huu za Rock City Marathon
kuboreshwa zaidi ukilinganisha na miaka
iliyotangulia, wawakilishi wa wanariadha na viongozi mbali mbali watapata fursa
ya kuzungumzia changamoto zinazokumba mchezo wa riadha nchini na jinsi ya
kukabiliana nazo.
“Tuko tayari
kwa mbio za Rock City Marathon 2014, zitakazofanyika Oktoba 26. Kamati ya
Maandalizi imeweka mikakati mizuri ili kuhakikisha mbio za mwaka huu zinakuwa
bora na zenye mafanikio kulinganisha na misimu iliyopita,” alisema Bi. Grace.
Mratibu huyo
alisema kuwa kwa kutokana na uendeshaji wa kuridhisha wa mbio hizo, wadhamini
wengi wamejitokeza kuwezesha kuzifanya mbio hizo kuwa bora zaidi mwaka huu.
“Baada ya
kufanya maandalizi ya Rock City Marathon kwa mafanikio kwa miaka tano mfululizo
na kuweza kupandisha kiwango chake, makampuni na mashirika mengi yamejitokeza
kudhamini mbio za mwaka huu kwa lengo la kuiboresha zaidi. Miongoni mwa
wadhamini wetu mwaka huu ni pamoja na NSSF, TSN Group, African Barrik Gold,
IPTL, TTB, TANAPA, New Mwanza Hotel, Nyanza Bottling Company, Sahara
Communications, New African Hotel, Continental decoders, ATCL, PPF, Umoja
Switch, and Bank M,” alisema Bi. Grace.
Rock City
Marathon zinaandaliwa na Kampuni ya Capital Plus International (CPI), kwa
ushirikiano na Chama cha Riadha Tanzania (RT), pamoja na Chama cha Riadha mkoa
wa Mwanza (MRAA), ambazo zimewavutia washiriki wengi wa ndani na nje ya nchi.
Bi. Grace
aliongeza kwamba, mbio hizo zitakuwa na vipengele vitano kwa msimu huu, ambavyo
ni mbio za kilometa 21 (wanawake na wanaume) na zile za kilometa tano kwa
wakimbiaji kutoka makampuni mbalimbali, kilometa tatu kwa watu wenye ulemavu,
kilometa tatu kwa watu wazima (zaidi ya miaka 55) na kilometa mbili kwa watoto
walio kati ya miaka 7 mpaka 10.
“Tunatarajia
watu wengi kujitokeza mwaka huu, kwa kuwa tumejipanga vizuri kwa msimu huu.
Tumejifunza kupitia mbio za mwaka jana, hivyo Kamati ya Maandalizi imekuja na
mpango madhubuti utakaoboresha mbio zetu kwa mwaka huu,” alisema Bi. Grace.
0 comments:
Post a Comment